NIDHAMU YA FEDHA NI NINI?
Nidhamu ya fedha ni sono muhimu sana katika maisha ya kila mtu uwe ni mfanyakazi, mfanya biashara, mkulima n.k ili kuweza kufanikiwa kiuchumi, haijarishi umeajiriwa, umejiajiri, unafanya biashara, mjasiriamali au mwanafunzi wa ngazi yoyote ya elimu. Kila jambo unalotaka kufanikiwa katika maisha yako linahitaji nidhamu ya hali ya juu sana, pia ili kufanikiwa kiuchumi (kifedha) huna budi kuwa na nidhamu ya hali ya juu katika matumizi ya fedha.
Mambo muhimu yanayohusiana na nidhamu ya fedha ni pamoja kuweka akiba, kupanga na kuishi kwa bajeti, kuwa na mipango yako ya kifedha katika maandishi, usimamizi wa fedha, taarifa za fedha, nk.
1. Ni uwezo wa kupanga na kutekeleza ulichopanga kufanya Kabla ya kupata pesa na baada ya kupata pesa. Ni uwezo wa akili ya mtu kutobabilisha mahitaji yasiyokuwa kwenye mpango wa bajeti mara tu anapopata pesa.
2. Ni msimamo wa mtu kuazimia kutotumia pesa vibaya au kutotumia pesa tofauti na mipango yake aliyojiwekea ili aweze kutimiza ndoto za mipango yake ya mafanikio aliyopanga kuifikia muda fulani ujao.
3. Nidhamu ya fedha ni utamaduni unaojengeka ndani ya mtu hatua kwa hatua mwaka hadi mwaka tangu akiwa mtoto mdogo na hudhihirika kivitendo akiwa mtu mzima atakapoanza kupata fedha zake mwenyewe.
4. Ni utamaduni unaomwezesha mtu kujizuia kufanya matumizi ambayo hakuyapanga mapema kabla ya kupata pesa.
5. Nidhamu ya fedha ni udhibiti wa ndani ya mtu mwenyewe (Self internal controls) anaokuwa nao mtu unaomwezesha binafsi kuheshimu fedha anazopata na kuzitumia kama alivyopanga tu.
6. Nidhamu ya fedha ni hulka aliyonayo mtu ndani yake inayomwezesha kujilinda na kujitambua kiasi kwamba hawezi kupelekeshwa na tamaa juu ya jambo fulani linalohusu matumizi ya pesa.
7. Nidhamu ya fedha ni tabia ya mtu kutii na kuheshimu bajeti yake binafsi, bajeti ya familia au taasisi, kuanzia awapo na fedha ndogo au akiwa na fedha nyingi sana kuanzia ngazi ya familia hadi ngazi za juu za taasisi zenye fedha nyingi.
Kuna mwandishi mmoja anajulikana kwa jina la Christopher Mwakasege aliwahi kuandika katika moja ya kitabu chake kuwa "Maamuzi unayoyafanya juu ya fedha ipitayo mikononi mwako ndiyo chanzo cha umasikini wako au utajiri wako" nidhamu ya fedha ni nyenzo muhimu sana katika mafanikio ya kiuchumi.
